JWTZ wadaiwa kuwateka Raia Huko Mtwara.


Mtwara/Dar. Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mkoani Mtwara wanadaiwa kuwakamata vijana wanne na kuwapeleka kusikojulikana juzi jioni kisha jana kuwafikisha Kituo cha Polisi Mkoa wa Mtwara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alikiri kukamatwa kwa watu hao: “Ni kweli tunawashikilia na tunahoji pande hizo mbili; yaani wananchi na wanajeshi kujua ukweli uko wapi.”
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Meja Eric Komba alisema hana taarifa hizo... “Kama ni kuteka JWTZ haliteki wananchi na kama ni kukamatwa, mimi sina taarifa ya maandishi wala ya mdomo, ndiyo kwanza nasikia kwako. Nitafute kesho nitakuwa nimeshafuatilia.”
Akizungumza kwa simu jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema tukio hilo lilitokea juzi saa kumi na moja jioni wakati vijana hao pamoja na watu wengine walipokuwa wakiangalia Kongamano la Amani nchini lililokuwa likirushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha ITV.
“Makundi ya wananchi yalikuwa yanafuatilia kongamano pale Mtwara. Wale vijana walikuwa kwenye grocery iitwayo Kwatelela inayotazamana na lango kuu la Mamlaka ya Bandari. Walishangilia kwa nguvu kuunga mkono baadhi ya hoja zilizotolewa kwenye kongamano. Karibu yao alikuwapo askari wa jeshi aliyevalia kiraia ila hawakujua hilo,” alisema Mtatiro na kuongeza:
“Kongamano lilipokaribia kwisha, askari yule aliwatolea bastola na kuwaweka chini ya ulinzi. Alipiga simu kuwaita wenzake na mara gari la jeshi lilifika wakachukuliwa.”
Mtatiro alisema amepata taarifa hizo baada ya kupigiwa simu na mashuhuda wa tukio hilo juzi jioni.
“Nimezungumza na mashuhuda wanne ambao wao wamenusurika baada ya kuwa mita chache katika eneo la tukio.” Mtatiro aliwataja vijana hao kuwa ni Ismail Nduva, Boniface Mkamale, Ismail Namwindula na Rashid Mniyanda.
Katika kongamano hilo ambalo lilihudhuriwa na wasomi, wanasiasa na viongozi akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi,
Serikali ilitupiwa lawama katika masuala mbalimbali hasa utendaji wa Jeshi la Polisi lakini pia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alilinyooshea kidole JWTZ kutokana na kuandamwa na tuhuma za utesaji na ubakaji huko Mtwara.
Hata hivyo madai hayo yalipingwa vikali na Brigedia Jenerali Elias Athanas aliyekuwapo katika kongamano hilo akisema: “Naomba kuweka wazi kuwa jeshi letu huko Mtwara, lina adabu na vitendo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa ni vya propaganda tu kama alivyosema Dk Slaa.”

Source: Mwananchi

Join Swahili One Community, "Like" and you will be one of us forever

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
Copyright © 2013. swahili one Blog - All Rights Reserved
Customized by: Grace Tommy The One | Powered by: BS
Designed by: Creative Blogger