Marekani yatuhumiwa kufuatilia kwa siri mawasiliano ya simu ya mkononi ya kansela wa Ujerumani.
Kwenye headlines za dunia sasa hivi miongoni mwa stori kubwa ni hii ya madai ya Ujerumani kwamba Marekani imekua ikifatilia kwa siri mazungumzo ya simu ya kiongozi wa Ujerumani, Kansela Angela Merkel ambapo kwa mujibu wa DW Swahili, Ujerumani imemuita balozi wa Marekani nchini humo John B. Emerson kuzungumzia madai hayo ya Idara ya usalama wa kitaifa ya Marekani kuyafatilia mawasiliano ya simu ya mkononi ya kansela.
Habari hii imekuja wakati Merkel na viongozi wengine wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kwa mkutano ambao unaonekana utagubikwa na habari za mawasiliano ya siri yanayodaiwa kufanywa na Marekani kwa washirika wake ambapo waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere aliliambia shirika la habari la ARD Ujerumani kwamba iwapo madai haya yatathibitishwa kuwa ya kweli basi litakuwa ni jambo baya sana.
De Maiziere amesema Marekani itabakia kuwa rafiki wa Ujerumani lakini jambo linalodaiwa kufanywa sio sahihi kabisa baada ya kupokea taarifa kwamba Marekani ilifatilia mawasiliano ya kansela Angela Merkel , hatua iliomfanya Merkel mwenyewe Jumatano kumpigia simu mara moja rais wa Marekani Barack Obama kutaka ufafanuzi zaidi kwa sababu aliamini kuna siku mawasiliano yake yatafatiliwa lakini sio na Marekani.
Baada ya haya madai ya Ujerumani, Marekani imekanusha kwa kusema haijayachunguza mawasiliano ya Kansela na haiwezi kufanya hivyo kamwe.
Haya madai yalitolewa kwa mara ya kwanza na mfanyakazi wa zamani wa idara ya kitaifa ya usalama nchini Marekani, NSA, Edward Snowden yaliyochapishwa na jarida la habari la Ujerumani, Der Spigel na sasa yameanza kuleta uhusiano mbaya kati ya Marekani na mataifa ya Ulaya yaliyokasirishwa na habari hizo za kufanyiwa uchunguzi wa siri na mshirika wao.
Mpaka usiku wa October 24 2013, taarifa mbalimbali ziliripoti kwamba mpaka sasa imefahamika ni viongozi wa nchi 35 kubwa wameshafatiliwa kwenye mawasiliano yao ya simu za mkononi bila wenyewe kufahamu.