AZIMIKA MTARONI BAADA YA KUNYWA MIZINGA MINNE YA "KONYA"
AMA kweli pombe si chai! Njemba mmoja, Mwala Kibodi a.k.a Chegge (22) amejikuta akiwa ‘amevurugwa’ na kuzimia mtaroni baada ya kudaiwa kunywa mizinga minne ya pombe kali aina ya ‘konya’ au ‘ngumu kumeza’.
Tukio hilo la aibu lilijiri Sinza-Lion, Dar wikiendi iliyopita ambapo Mwala alikutwa na wapita njia waliomtambua kuwa ni fundi makenika katika gereji moja iliyopo maeneo hayo.
Wakiwa kazini, vijana wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) kwa kushirikiana na raia wema, walianza kumpaka ndimu kama huduma ya kwanza ambapo hakuonesha kuzinduka hivyo walimpeleka polisi kisha kuchukua fomu ya matibabu (PF3) na kupelekwa Hospitali ya Sinza-Palestina kwa matibabu.
Akizungumza na OFM, mmoja wa watu walioshuhudia tukio zima kwa sharti la kutotajwa jina, alisema Mwala ‘alizima’ kuanzia usiku wa jana yake mishale ya saa mbili mpaka siku hiyo bila kuzinduka, hali iliyowatia wasiwasi wakihofia huenda mtu huyo angeweza kupoteza uhai katika maeneo yao.
Akizungumza na paparazi wetu, rafiki wa karibu wa Mwala, Ramadhan Tito alisema kuwa awali jamaa huyo alikuwa akibishana na rafiki zake kwamba anaweza kumaliza mizinga minne ya pombe kali, jambo ambalo wenzake walimbishia.
Rafiki huyo alitiririka kuwa kwa kuthibitisha kwamba anao uwezo wa kufanya hivyo, Mwala alizifakamia pombe hizo kwa sifa hadi kuzimaliza.
Rafiki huyo alidai kuwa hadi wanaachana na Mwala usiku ule, hakuwa na dalili zozote kama asingeweza kufika nyumbani kwake, Mabibo, Dar.
Hadi OFM wanaondoka hospitalini hapo, Mwala alikuwa akiendelea na dozi ya kuondoa pombe mwilini. Ulevi noma sana!
GPL.