Mwanafunzi Ashikiwa Uchawi, Akutwa na zana kibao za uchawi huku akiwa na Nguo ya Ndani Tu!!!
Stori:Gladness Mallya na Haruni Sanchawa
AMINI usiamini, duniani kuna uchawi! Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Pasco (21) ambaye pia ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Samaritan iliyopo wilayani Rorya mkoani Mara amekutwa getini kwa kaka’ke, Edward Raphael akiwa amefungwa kamba na matunguri.
Kwa mujibu wa mashuhuda, Pasco alikuwa amefungwa kamba mikononi na miguuni huku akiwa na nguo ya ndani pekee.
Habari zilieleza kuwa pia kijana huyo alikuwa amepakwa unga na kuandikwa maandishi ya Kiarabu mwilini huku kiunoni akiwa na shanga, hali iliyowashangaza wengi.
Akizungumza na wanahabari wetu juu ya tukio hilo, kaka wa kijana huyo alisema tukio hilo lilitokea siku ya Jumapili, wiki mbili zilizopita ambapo aliamka na kujiandaa kwa ajili ya kwenda kwenye shughuli zake lakini alipofungua geti alishangaa kumuona mtu akiwa amelala akiwa hajitambui.
Alisema baada ya tukio hilo, alirudi ndani haraka na kumwita mpangaji wake ili akashuhudie alichokiona.
Mazagazaga aliyo kutwa nayo
Alisimulia kuwa baada ya mpangaji huyo kuamka, waliamua kwenda polisi lakini wakiwa huko, mkewe aliamua kwenda kumchunguza mtu huyo kwa makini usoni ambapo aligundua kuwa ni shemeji yake, jambo ambalo lilizidi kuwachanganya watu.Alisema aliporudi alikuta umati mkubwa wa watu umemzunguka Pasco.
Kaka mtu alisema kuwa alitimba na askari ambao walimfungua kamba na safari ya kuelekea kituo cha polisi ikaanza lakini wakiwa njiani, kijana huyo alikuwa akiongea maneno ya ajabu kama vile mtu mwenye majini.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Nyumba Kumi, Shina la Mube, Joseph Paja alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema naye alikuwa miongoni mwa mashuhuda.
Alisema kuwa alipofika, alikuta kijana huyo aliyewahi kuishi mtaani hapo kwa kipindi kirefu akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi, hali ambayo ilimshangaza kila mtu.
Mchungaji wa Kanisa la Church of World, Steven Paul ambaye naye alishuhudia tukio hilo, alisema kuwa baada ya ndugu kuamua kumpeleka polisi aliambatana nao hadi kituoni lakini walipofika, askari walimtema kwa kigezo kuwa hakuwa na kesi ya kufunguliwa, wakashauri apelekwe hospitali.
Ilielezwa kuwa zoezi la kumpeleka hospitali lilifanyika lakini walipofika huko, madaktari walimkataa kwa kigezo kuwa hawakuona ugonjwa wowote, jambo lililosababisha hofu kutanda.
Akizungumza na waandishi wetu, mchungaji huyo alisema kutokana na kote huko kushindikana, aliamua kumchukua kijana huyo na kuishi naye nyumbani kwake kwa lengo la kumfanyia maombi.
Baada ya kumchukua, alianza dozi ya maombezi ya nguvu ambapo hivi sasa anaendelea vizuri.
Katika mahojiano na waandishi wetu, Pasco alisema hajui kilichotokea hadi akajikuta amefika Dar, tena getini kwa kaka yake akiwa uchi.
Alisimulia kuwa siku hiyo, alienda benki kutuma ada ya shule na baada ya hapo, alirudi nyumbani kwa bibi yake na kumkuta akiandaa ugali ambapo alikula kidogo kwani alikuwa akihisi maumivu makali ya kichwa.
Baada ya kushindwa kula vizuri, bibi yake alimtaka ale chungwa ambapo alichukua moja na kwenda nalo chumbani, akachukua panga kisha kulikata vipande viwili lakini alipoanza kula, kabla ya kumaliza kipande kimoja alihisi usingizi mzito ambapo alikuja kushtukia akiwa sehemu tofauti yaani getini kwa kaka yake akiwa amezingirwa na watu kibao.
Alieleza kuwa kutokana na kusumbuliwa na mauzauza ya kichawi ndiyo sababu kubwa iliyomfanya kaka yake amhamishie Rorya mkoani Mara ambako alienda kuanza kidato cha pili wakati huku Dar alikuwa ameshafika kidato cha nne.
Chanzo: GPL