Bondia wa Tanzania Azamia Nchini Australia alipoenda katika Pambano
Miaka Saba iliyopita mabondia wawili wa Tanzania walizamia Australia wakati wa michuano ya Jumuiya ya Madola 2006
Dar es Salaam. Bondia wa Tanzania, Jonas Segu anadaiwa kuzamia nchini Australia alipokwenda kwenye pambano hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Anthony Rutta ambaye ni mmoja wa viongozi wa Chama cha Ngumi Tanzania (PST) iliyotoa kibali kwa bondia huyo kupigana nchini Australia, baada ya pambano hilo Segu alitokomea kusikojulikana.
“Segu alikwenda nchini humo kucheza pambano na Luke Sharp lililofanyika kwenye Ukumbi wa Metro City, Jimbo la Northbridge, na Segu kupigwa kwa Knock out (KO) raundi ya tano kwenye uzani wa light welter.
“Muda mfupi baada ya pambano na Segu kulipwa fedha zake hakuonekana tena na hakuwa kwenye msafara wa wachezaji waliokuwa kwenye msafara huo waliorudi nchini,” alisema Rutta.
Alisema baadaye alipewa taarifa na mkuu wa msafara huo, Obote Ameme aliyedai bondia huyo kubaki Australia.
Alisema mabondia wengine walioambatana na Segu, Japhet Kaseba na Ibrahim Maokola ambao walikuwa miongoni mwa mabondia wa Tanzania waliocheza nchini humo tayari wamewasili nchini.
Kwa mujibu wa Ameme, baada ya pambano hilo mabondia wote walirudi hotelini kupumzika na asubuhi ya siku iliyofuata Segu hakuonekana kwa ajili ya safari ya kurudi nyumbani, walijaribu kumtafuta kila sehemu bila mafanikio na kujaribu kutoa taarifa kwenye redio nchini humo bila mafanikio yoyote.
Hiyo ni mara ya pili kwa mabondia wa Tanzania kuzamia nchini Australia, mwaka 2006, mabondia, wawili, Omary Kimweri na Karim Matumla walizamia nchini humo walikokwenda na timu ya Tanzania kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika mjini Melborne.