Bado Mvutano kuhusiana na Mashine za EFD za TRA, Nani amesababisha Haya?!!
Mamlaka ya Mapato Tanzania iko katika msuguano na wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na mamlaka hiyo kuanzisha mfumo mpya wa utoaji stakabadhi za kielektroniki kwa kutumia mashine ziitwazo EFD.
Ugomvi mkubwa wa wafanyabiashara hao unatokana na bei inayodaiwa ni kubwa ya kununulia mashine hizo, inayofikia Sh800, 000 kwa kila moja. Madai mengine ni kasoro za kiufundi za mashine hizo na kitendo cha TRA kutumia mzabuni mmoja kuingiza mashine hizo.
Jana mvutano huo ulipiga hodi katika eneo maarufu kibiashara la Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo wafanyabiashara waligoma kufungua maduka kama ambavyo wamekwishafanya wenzao katika mikoa ya Mbeya na Morogoro.
Pamoja na ufafanuzi wa TRA kwamba baada ya majadiliano na wafanyabiashara bei za mashine za EFD zimepungua hadi Sh600, 000 kwa kila moja, bado muafaka kamili haujafikiwa.Tunaafikiana na ushauri unaotolewa na TRA kwamba mvutano huo umalizwe kwa amani kwa njia ya mazungumzo na majadiliano baina ya mamlaka hiyo na wafanyabiashara badala ya njia waliyoichagua ya migomo na maandamano.
Tunaishauri TRA iendelee kutoa majibu sahihi na kusisitiza umuhimu wa mashine hizo, huku ikitambua kwamba hakuna mfanyabiashara anayelipa kodi akicheka, hivyo iwe imara kusimamia mfumo huo mpya bila kuingiza ujanja ujanja unaoweza kuikwamisha.
Kinachojitokeza bayana hapa ni kuwapo mawasiliano hafifu baina ya TRA na wafanyabiashara. Kwa mfano, wafanyabiashara bado wanadhani ni kampuni moja tu iliyopewa tenda ya kusambaza mashine hizo, wakati ni kampuni 11 zilizopewa tenda hiyo. Hakika, tatizo ni mawasiliano na TRA lazima ikiri udhaifu huo na kuchukua hatua stahiki.
Uanzishaji wa mashine za EFD ni mkakati sahihi wa ukusanyaji na usimamizi wa kodi, hasa katika maeneo ambayo TRA haikuwa inayafikia. Ni uamuzi ambao utaliwezesha Taifa letu kupata fedha za kutosha kujenga miundombinu na kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Tunashawishika kuamini kuwa, hata mafanikio ambayo TRA iliyaeleza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Mlipakodi ya kuimarika kwa ukusanyaji mapato kutoka Sh4,049.1 trilioni mwaka 2008/09 hadi Sh7,739.3 trilioni mwaka 2012/13, yamesaidiwa na mashine hizo.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukikemea uzembe na usimamizi mbovu wa kodi uliosababisha maofisa wa TRA kuacha fedha nyingi zikilala kwa wafanyabishara wa kati, badala yake kila kukicha wakawa wanakimbilia makusanyo ya kuokota yanayotokana na mishahara ya wafanyakazi.
Kwa mfano, tumewahi kushauri kuwa vinahitajika vyanzo vipya vya mapato, kwa kuwatambua na kuwatoza wafanyabiashara wa kada ya kati katika maduka, baa, saluni, bucha za nyama, kumbi za starehe na harusi na maeneo kama hayo.
Mbali na kuongeza mapato, pia tunadhani Serikali ingefanya juhudi za kuziba matundu na mianya ya uvujaji wa mapato yake ili kuhakikisha kila kinachokusanywa kinaelekezwa katika maendeleo ya nchi na wananchi, badala ya kutafunwa na mchwa wasiojali masilahi ya umma.
Hatuna shaka kwamba TRA ikijipanga inaweza kukusanya mapato zaidi, hasa ikisimamia vizuri uamuzi wake wa kutumia EFD nchini kote na kuweka utaratibu wa kudumu wa kufuatilia kwenye maduka kuona iwapo wanatoa risiti hizo au la, maana tayari kuna madai kuwa wateja wanatakiwa kuchagua kati ya kuuziwa bidhaa kwa bei ndogo bila risiti au kwa bei kubwa na risiti za kielekroniki.
Mananchi.