MZEE WA KANISA ALIFUNGA KANISA! HUKO MBEYA
WAUMINI wa Kanisa la Nyumba ya maombi (House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship) lililopo jijini Mbeya wamekosa sehemu ya kufanyia ibada baada ya Kanisa lao kufungwa na mzee wa Kanisa hilo, Laurence Malongo.
Mchungaji wa Kanisa hilo, Owden Mwakifuna amesema hivi karibuni mzee Mwalongo alifika kanisani na kuwataka waumini wote kutoka huku akionekana kutawaliwa na jazba.
Mchungaji Mwakifuna alisema kanisa hilo lilijengwa baada ya Malongo kutoa uwanja kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo kama shukrani baada ya kufanyiwa maombi yeye na mwanawe na kupona magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua.
Baada ya kanisa hilo kufungwa Mchungaji Mwakifuna alitoa taarifa kwa kiongozi wa kanda ya Mbeya, Mchungaji Isaya Laiser na kufanya vikao vya mara kwa mara ili kutatua mgogoro huo bila mafanikio.
Kufungwa kwa kanisa hilo lililopo kata ya Itezi kumewafanya waumini kutembea kilometa 10 hadi makao makuu ya kanda eneo la Pambogo Kata ya Iyela jijini Mbeya.
Baada ya kufungwa kwa kanisa hilo, viongozi wa waumini hao waliandikia barua uongozi wa kata ambao uliitisha kikao Desemba 5 mwaka huu.
Kikao hicho chini ya Diwani wa Kata ya Itezi, Frank Mayemba ambaye alisema kiwanja hicho ni mali ya Malongo na hati yake haijabadilishwa.
Kikao kilimalizika kwa Malongo kuchukua viti 60 na kulifunga jengo hilo mbele ya uongozi wa kata ya Itezi na kuamriwa maandishi ya kanisa hili yafutwe kwenye kuta za jengo hilo mara moja.