Ripoti kuhusu Mishahara ya Vigogo, Ipo Juu kulingana na Ufanisi wao.
Ripoti mpya ya utafiti imebainisha kuwa mishahara mikubwa wanayolipwa viongozi wa juu serikalini na wanasiasa hailingani na utendaji wao wa kazi.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana jijini Dar es Salaam, imeeleza kuwa viongozi hao wanalipwa mishahara inayotofautiana kwa kiwango kikubwa na pato la mwananchi wa kawaida.
Huku ikitaja mapato ya mishahara ya marais wa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, imesema kuwa hali hiyo ni kuibebesha jamii mzigo wa kugharimia malipo ya viongozi.
Akizindua ripoti hiyo iliyochunguza gharama za kuwalipa viongozi wa Serikali na wanasiasa, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa), Dk Theodore Valentine, alisema kuwa viongozi wa Afrika Mashariki ndio wanaoongoza kwa kulipwa mishahara mikubwa zaidi chini ya Jangwa la Sahara.
“Kama viongozi wakuu watakuwa wanalipwa mishahara mikubwa, nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zitaweza kugharimia demokrasia?” alihoji Valentine.
Utafiti huo uliofanyika kati ya mwaka 2009 na 2012, umebainisha kuwa Rais wa Tanzania analipwa mshahara dola 172,014 kwa mwaka (Sh275 milioni) sawa na Sh22.9 milioni kwa mwezi, huku Rais wa Kenya, akiongoza kwa kulipwa dola 515,021 kwa mwaka (Sh824 milioni) kwa mwaka sawa na Sh68.6 milioni kwa mwezi.
Rais wa Rwanda analipwa dola 199,000 kwa mwaka (Sh124 milioni) sawa na Sh10 milioni kwa mwezi, wakati rais wa Nigeria akipokea dola 161,902 (Sh259 milioni) ambazo ni sawa na Sh21 milioni kwa mwezi.
Pia umeeleza kuwa Rais wa Kenya analipwa mara 320 zaidi ya pato la mwananchi wa kawaida wa nchi hiyo, wakati rais wa Afrika Kusini anapata mara 46 na Rwanda mara 150 zaidi ya mwananchi wa kawaida.
Ripoti hiyo imeendelea kubainisha kuwa rais wa Tanzania analipwa mara 8.2 ya mshahara wa hakimu, huku rais wa Kenya akipokea mara 13.1 na kumpita rais wa Rwanda anayechukua mara 12 zaidi ya mshahara wa hakimu.
Kwa upande wa wabunge, utafiti huo umeeleza kuwa wabunge wa Tanzania wanalipwa mara 3.0 ya mshahara anaolipwa hakimu, Kenya (5.5) na Rwanda (3.0). Viwango hivyo vimetajwa kuwa vikubwa kuliko vya wabunge wa Nigeria na Afrika Kusini.
Naibu Spika anena
Naye Naibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai alisema kuwa umefika wakati ambapo mishahara ya viongozi wa umma inabidi iwekwe wazi kwa wananchi.
“Ningependa mishahara ifahamike kama ilivyo kwa nchi nyingine, hii itaondoa uongo kwa wabunge,” alisema.
Alisema mishahara wanayolipwa wabunge siyo mikubwa na kwamba inapaswa kuongezwa zaidi kwa kuwa hivi sasa imetofautiana kidogo na ya wakuu wa wilaya.
“Mshahara wangu mimi kama Naibu Spika ni mdogo…, hata wa Waziri Mkuu siyo mkubwa. Siku zote mtu anapoongezewa mshahara inamwongezea motisha ya kufanya kazi,” alisema Ndugai.
Serikali yajibu
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga, alisema viongozi wanalipwa mshahara kutokana na nyadhifa walizonazo, hivyo haoni sababu ya jambo hilo kujadiliwa.
Alisema mshahara ni siri ya mfanyakazi husika, na kwamba iwapo itawekwa wazi baadhi ya watu wataacha kujadili mambo ya maendeleo na badala yake wataanza kuzungumzia malipo hayo.
“Tujadili kuhusu namna ambavyo gesi itatuletea maendeleo kwenye uchumi wa nchi yetu na siyo mishahara,” alisema.
Alipopigiwa simu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alihoji kuwa anazungumza na nani, mwandishi alipojitambulisha alitaka apewe muda hadi baadaye kwa madai kuwa hakuwa sehemu nzuri.
Rais Kikwete na OGP
Akinukuliwa na gazeti la Serikali, Rais Jakaya Kikwete, ambaye Oktoba 31 hadi Novemba Mosi 2013, alihudhuria Mpango wa Pamoja wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP) uliofanyika London, Uingereza, ambapo alizungumzia uwazi kwenye Serikali yake likiwemo suala la mishahara.
Mkutano huo ulihudhuriwa na washiriki 1,000 kutoka nchi 60 wanachama na Rais Kikwete alipata nafasi ya kuuelezea mkutano huo, namna Tanzania ilivyoanza utekelezaji wa masharti ya mpango huo.
Rais Kikwete alisema kuwa mshahara wa mtumishi wa umma hauwezi kuwa siri na ndiyo maana unawekwa katika bajeti ya serikali.
“Mishahara haiwezi kuwa siri. Si ipo kwenye bajeti za Serikali?” Alijibu Rais Kikwete alipoulizwa kama suala la mishahara litaendelea kuwa siri katika utekelezaji wa mpango huo.
Rais Kikwete alisema: “Changamoto iliyopo ni kwamba mpango huu unabadili mazoea yetu ya kufanya kazi. Sisi katika kila Serikali kila kitu kilikuwa siri. Sasa OGP inataka mambo haya yawe wazi, ifike hatua mtu aone kutoa habari ni wajibu.”
TUCTA yatoa kauli
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicolas Mgaya alisema wabunge wanalipwa mishahara mikubwa lakini baadhi yao hawaonekani kwenye vikao.
Alitaka mishahara yao iwekwe wazi kwa wananchi kwa kile alichokieleza kuwa kwa sababu wanalipwa kwa kutumia kodi za wananchi.
Anavyosema Profesa Wangwe
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samuel Wangwe alisema kuna haja ya kuangalia gharama za kuwalipia viongozi.
“Tuangalie gharama ya demokrasia, lakini jambo la msingi ni kuwa kama wabunge wanalipwa kiasi kinachotajwa basi wafanye kazi yao wanayostahili na wasisahau kwamba wanawawakilisha wananchi ambao ni maskini,” alisema.
Profesa Lipumba
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi - CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ni mchumi kitaaluma alisema kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa viongozi wakilipwa mishahara mikubwa wanafanya kazi zaidi.
“Hakuna ushahidi wowote kwamba kwa kuwalipa wabunge mishahara mikubwa basi wanafanya kazi vizuri zaidi,” alisema.
Akitolea mfano wabunge wa Kenya alisema: “Katika kipindi cha miaka mitano mbunge wa Kenya analipwa dola za Marekani dola 1milioni (sawa wa Sh1.6 bilioni) kiasi ambacho ni sawa na Sh26 milioni kwa mwezi.”
Aliongeza kuwa mishahara ya wabunge wa Tanzania ni zaidi ya mara 40 ya pato la kawaida la mwananchi.
Alipendekeza kuanzishwa kwa taasisi ambayo itapewa jukumu la kusimamia mapato ya viongozi wa umma, na kwamba ni vyema katiba izungumze kuwa mishahara na marupurupu ya wabunge itapangwa na taasisi ambayo ipo huru itakayozingatia mapato ya nchi yalivyo.
Mwananchi