Simba Wakwaa Kisiki, Mashabiki wafanya fujo kubwa.
MBIO za Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara zinazidi kuwa ngumu baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar jana, lakini habari mbaya zaidi ni kuwa mashabiki wa timu hiyo walijeruhiwa kutokana na vurugu zilizotokea kwenye mechi hiyo.
Vurugu hizo zilitokea katika mechi hiyo ambayo ilipigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya Kagera kusawazisha bao katika dakika ya 95 kutokana na mkwaju wa penalti uliopigwa na Salum Kanoni, mara baada ya beki wa Simba, Joseph Owino kumchezea vibaya Daudi Jumanne.
Mara baada ya bao hilo la kusawazisha, mashabiki wa Simba walianza kuvunja viti, kitendo kilichosababisha askari wa kutuliza ghasia kurusha mabomu mawili ya machozi kwenye jukwaa la mashabiki hao, ndipo mtifuano ukawa mkubwa.
Tukio hilo lilitokea sekunde chache kabla ya mwamuzi wa kati, Mohamed Theofile wa Morogoro kumaliza mchezo huo, ambapo askari waliendelea kurusha mabomu kadhaa.
Gazeti hili lilishuhudia viti zaidi ya 50 vikiwa vimevunjwa na kuzagaa, huku baadhi ya mashabiki wakiumia na wawili kupoteza fahamu, huku wachezaji wakitoka mbio kuelekea vyumbani mara baada ya kipenga cha mwisho.
Mmoja wa mashabiki aliyepoteza fahamu ni wa Simba aliyetambulika kwa jina la Fii Kambi, ambaye hali yake ilikuwa mbaya lakini baada ya kupatiwa huduma ya kwanza na wahudumu wa Msalaba Mwekundu, alirejewa na fahamu, lakini mpaka gazeti hili linaondoka uwanjani hapo, alikuwa bado hajarejea katika hali yake ya kawaida.
Akizungumzia juu ya kilichotokea uwanjani hapo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’, alisema:
“Tumeingiwa na hofu na yawezekana tunatengenezewa mazingira magumu ya kutwaa ubingwa kutokana na kuonewa.”
Upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope, alisema: “Asilimia kubwa ni matatizo ya waamuzi wetu wa Tanzania, aliongeza muda mwingi wakati dakika zilikuwa zimemalizika.”
Naye nahodha wa Simba, Said Nassoro ‘Chollo’ naye alisema: “Kitendo cha mabomu kulipuliwa wakati tukiwa uwanjani mechi ikiendelea ni jambo baya na wanatakiwa kulichukulia hatua kali.”
Katika mechi hiyo Simba ndiyo ilianza kupata bao katika dakika ya 45 kupitia kwa Amissi Tambwe ambaye ameendelea kuwa kinara wa mabao kwa kufikisha mabao tisa na kumzidi Hamis Kiiza wa Yanga mwenye mabao nane.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni, akisema: “Naishauri TFF mpya iangalie juu ya suala la waamuzi kwa kuwa wao ndiyo tatizo.”
Upande wa Kocha wa Kagera, Jackson Mayanja, alisema: “Mwamuzi alifanya kazi inavyotakiwa kwa kuwa aliona mchezaji alifanyiwa faulo, ndiyo maana akatoa penalti halali.”
Kituko katika mchezo huo, ni mashabiki wa Simba kushangilia uamuzi wa Abel Dhaira kuwekwa benchi katika mechi, badala yake langoni akasimama Abuu Hashim ambaye alidaka dakika zote 90.
gpl