ZITTO AVULIWA CHEO CHA USEMAJI WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI
Mambo yanazidi kumwendea kombo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe baada ya kuvuliwa rasmi cheo cha Naibu Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Katibu wa wabunge wa Chadema, David Silinde, alithibitisha jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu Kambi Rasmi ya Upinzani kumvua cheo hicho Zitto na kwamba tayari taarifa imeshapelekwa kwa spika.
“Ni kweli tulikutana leo mchana na tumeamua kumvua rasmi cheo cha Naibu Msemaji wa kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na sasa nafasi hiyo iko wazi,” alisema Silinde.
Silinde alisema uamuzi huo umefikiwa ikiwa ni kutekeleza maagizo ya Kamati Kuu ya Chadema iliyoamua Zitto kuvuliwa nyadhifa zote ndani ya chama kutokana na kudaiwa kukisaliti chama hicho.
Kwa mujibu wa Silinde ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, alisema hatima ya uanachama wa Zitto pamoja na Ubunge wake sasa iko mikononi mwa Kamati Kuu ya Chadema. Zitto tayari amekata rufani Baraza Kuu la chama hicho kupinga hatua ya Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake hizo.