Rais wa Madagascar awasili Nchini, Kujadili kuhusu mgogoro wa amani wa kisiwa hicho.
Dar es Salaam. Rais wa Serikali ya Mpito ya Madagascar, Andry Rajoelina amewasili nchini kwa ziara ya kikazi na jana alitarajiwa kuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Rais Rajoelina alilakiwa na Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC-Troika) ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa asasi hiyo, Rais Kikwete ndiye aliyepewa jukumu na viongozi wenzake wa nchi wanachama wa SADC, kutafuta suluhisho la mgogoro wa kisiasa katika Kisiwa cha Madagascar.
Viongozi hao wawili walikutana Ikulu, kuzungumzia hali ya kisiasa nchini Madagascar ambapo Rais Kikwete alimweleza Rais Rajoelina matokeo ya kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa SADC-Troika, kilichofanyika chini ya uenyekiti wake, Jumamosi usiku, mjini Pretoria, Afrika Kusini.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI