Serikali yatangaza kuvihamisha vituo vya dala dala vya Ubungo na Mwenge jijini Dar
VITUO vya daladala vya Ubungo na Mwenge vinahamishwa kupisha Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), ambao miundombinu yake inaendelea kujengwa.
Kituo cha Ubungo kitahamishiwa nyuma ya jengo la Mawasiliano lililopo Barabara ya Sam Nujoma, vivyo hivyo kituo cha Mwenge, kitatumika kwa ajili ya kushusha abiria pekee.
Ofisa Habari wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera amesema, magari ya Mwenge, yatakuwa na uamuzi wa ama kuishia kwenye stendi ya Makumbusho ;au kwenda hadi kituo hicho kitakachohudumia magari ya Ubungo kilichoko Mawasiliano.
Kwa mujibu wa Mhowera, wakati wowote kuanzia sasa vituo hivyo, vitabomolewa kupisha mradi huo.
Hata hivyo, hakuelezea kwa undani juu ya maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho kipya. Alisema hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi, kuhusu hatua zinazochukuliwa na manispaa, kuwezesha wafanyabiashara ndogo kupata maeneo ya kuendesha shughuli zao.
Alisema baada ya kituo cha Ubungo kuhamishiwa katika eneo hilo jipya, hakutakuwa na mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuuza bidhaa zozote kama ilivyo sasa.
Alisema kuhamishwa kwa vituo hivyo, kutatoa nafasi kwa wafanyabiashara kwenda katika maeneo waliyopangiwa kwa kuwa hakutakuwa na nafasi, kwani yote yatatumika kwa ajili ya barabara.
“ Kwa hiyo ni bora wakaanza kujiondosha wenyewe mapema kabla hatua ya kuondolewa na ujenzi kuwafikia,” alisema.
Kwa mujibu wa ofisa habari huyo, yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kazi hiyo katika masoko mbalimbali likiwemo laKijitonyama.
-Habari leo