ACHOMWA KISU NA KUPOOZA BAADA YA KUKATAA KUMNUNULIA JAMAA POMBE
KATIKA hali ya kushangaza, mwanaume mmoja, Maige Masyome (29) amechomwa kisu na mwenzake, Amosi Anthony kwa kosa la kukataa kumnunulia pombe ya kienyeji, tukio lililotokea Novemba 10, mwaka huu, Kigonga, Nyamunge mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wetu akiwa hoi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Maige alisema siku ya tukio alikutana na Amosi kwenye kilabu cha pombe ya kienyeji maarufu kama Kwa Mama Mung’ori ambapo mwenzake huyo alimtaka amnunulie pombe lakini akakataa.
Alidai Amosi alibadilika na kuanza kumlazimisha na alipozidi kukataa alinyamaza lakini wakati akiinuka kuondoka zake eneo hilo, Amosi alimchoma kisu shingoni.
“Nilishangaa baada ya kuona anazidi kunizonga nimnunulie pombe, nilipokataa akakaa kimya. Sasa wakati nainuka nilishangaa jamaa anasimama na kunichoma kisu shingoni,” alisema Maige kwa taabu.
Kwa upande wake, kaka wa mgonjwa huyo aitwaye Wambura, alisema walifungua kesi katika Kituo cha Polisi cha Nyamango kwa jalada NYM/RB/3291/2013 na kuongeza kuwa wamepata taarifa kuwa mtuhumiwa bado yupo uraiani akitembea bila wasiwasi wakati ndugu yao anateseka hospitali.
“Nimepata taarifa kuwa mtuhumiwa anatembea bila wasiwasi mtaani wakati mdogo wangu anateseka hapa ndani. Ninaomba mtuhumiwa akamatwe ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Wambura.
Hadi sasa Maige amelazwa katika Hospitali ya Bugando akiendelea na matibabu huku akiwa amepooza sehemu ya mwili wake kuanzia kifuani hadi miguuni.
GPL