Dk Mvungi Apelekwa Afrika Kusini kwa Matibabu zaidi.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi, amepelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi kutokana na kujeruhiwa na majambazi.
Dk Mvungi aliondoka nchini saa 6.15 mchana jana kwa kutumia ndege maalumu ya kubebea wagonjwa aina ya Citation 560, Medevac kuelekea jijini Johannesburg, Afrika Kusini ambako atatibiwa katika Hospitali ya Milpark.
Ndege hiyo pia ndiyo ilitumika kuwasafirisha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka na Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, Absalom Kibanda wakati waliposhambuliwa na watu wasiojulikana kwa nyakati tofauti.
Akizungumza muda mfupi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuwa imebidi wamsafirishe nje ya nchi, ili kurahisisha matibabu yake.
“Hali yake siyo mbaya sana na anapumua mwenyewe, lakini tumeona tumhamishie Afrika Kusini ambako kuna huduma na vifaa vya uhakika,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Tunawashukuru Moi (Taasisi ya mifupa ya Muhimbili) wamejitahidi, lakini tumeona tumhamishie Hospitali ya Milpark ili apate msaada zaidi. Watanzania waendelee tu kumwombea,” alisema.
Mbatia pia amelitaka Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi wake, ili kuwabaini watu hao na sababu ya kumdhuru Dk Mvungi.
Hali kadhalika kuchunguza mazingira ya kuibiwa kwa kompyuta na simu yake.
“IGP amenihakikishia kuwa watachunguza, lakini, tunataka polisi wa `speed up’ (waharakishe) uchunguzi wao. Tujue lengo la watu hao kuchukua kompyuta na simu yake, maana zilikuwa na taarifa nyingi. Tunachohitaji ni ufanisi,” alisisitiza Mbatia.
Mbatia amewashukuru Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad na viongozi wa vyama vya siasa na taasisi za kidini, kwa kumtembelea na kumjulia hali Dk Mvungi alipokuwa hospitalini.
Katika uwanja wa ndege, alikuwepo pia Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Asaa Mohamed pamoja na ndugu wa Dk Mvungi.
Katika safari hiyo, Dk Mvungi ameambatana na daktari wake Clement Mugisha kutoka Moi.