Operesheni Ujangili yasimama kwa muda.
Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali imesitisha kwa muda Operesheni Tokomeza Ujangili ili iweze kujipanga upya.
Akilihutubia Bunge Mjini Dodoma jana, Rais Kikwete alisema uamuzi wa kuendesha operesheni hiyo ulikuwa sahihi kutokana na historia ya ujangili nchini, lakini kutokana na malalamiko yaliyoibuka baada ya operesheni hiyo kuanza yameilazimu kusitisha kwa muda.
Tangu kuanza kwa operesheni hiyo, kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wabunge, wanaharakati na wananchi dhidi ya askari waliokuwa wakiiendesha yakiwamo ya watu kujeruhiwa, kuchomewa nyumba, mifugo kuuawa, kupigwa na uporaji.
Operesheni hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa pamoja na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa).
Operesheni hiyo ilizuiwa baada ya suala hilo kutinga bungeni na watunga sheria hao kuweka kando tofauti zao za kiitikadi na kuungana wakitaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Mathayo David Mathayo wawajibike.
Rais Kikwete alisema hakukasirishwa na maoni ya wabunge kuhusu kuwapo kwa kasoro za utekelezaji wa operesheni hiyo iliyolenga kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori.
Alisema Tanzania ilikuwa na tembo 350,000 wakati inapata uhuru mwaka 1961 kabla ya ujangili kuibuka kati ya miaka ya 1970 na 1980.
Alisema sensa iliyofanyika mwaka 1989 ilibaini kubaki kwa tembo 55,000 tu nchini wakati Tanzania ilikuwa ikiongoza kwa idadi kubwa ya wanyamapori hao.
“Baada ya hapo Serikali ilianzisha Operesheni Uhai iliyoongozwa na Kamanda wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Meja Jenerali John Walden ambaye ametangulia mbele za haki dhidi ya majangili. Tulifanikiwa kwani mwaka 2009 ilipofanyika sensa ya wanyama, ilibainika tembo walikuwa 110,000,” alisema.
Alisema baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya la ujangili wa meno ya tembo... “Kati ya mwaka 2010 hadi Septemba 2013, meno ya tembo yaliyokamatwa ni 3,899 yenye uzito wa kilo 11,212. Pia vilikamatwa vipande 22 vya meno vilivyochakatwa kuwa fimbo na urembo ambavyo vilikuwa na uzito wa kilo 3,978.” Alisema pia vilikamatwa vipande 4,692 vya meno ya tembo vikiwa vimetoroshwa nje ya nchi vikiwa na uzito wa kilo 17,797... “Hapo unazungumzia zaidi ya kilo 36,000, sawa na zaidi ya tembo 15,000.
“Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa kulingana na manufaa yaliyopatikana katika operesheni zilizopita. Tusipochukua hatua ni sawa na kuwapa kibali majangili kuua tembo. Wanyama watakwisha na historia itatuhukumu vibaya.”
Alisema Serikali itazingatia maoni ya wabunge kuhusu operesheni hiyo na kurekebisha dosari zilizojitokeza. “Serikali itachukua hatua dhidi ya watendaji wasiokuwa waadilifu na wasiokuwa waaminifu wataondolewa, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tukianza upya operesheni itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa,” aliongeza.