Bastola ya Vai ni halali kwake kisheria - Polisi
Arusha. Polisi mkoani hapa, imetoa ufafanuzi kuhusu silaha aina ya bastola iliyokuwa ikitumiwa na mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, Vailet Mathias (37), aliyepigwa risasi na polisi Octoba 31,mwaka huu kuwa ni mali yake.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi wa mkoani hapa, Liberatus zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na jijini hapa kuwa, bastola hiyo ni mali ya kigogo mmoja wa Serikali jina linahifadhiwa.
“Ninachoweza kusema,bastola aliyokuwa nayo huyo dada ni mali yake halali na aliipata kwa kufuata taratibu zote,” alisema Kamanda Sabas.
Alisema hata hivyo, polisi mkoani Arusha bado inafanya uchunguzi wa tukio la kupigwa risasi mfanyabiashara huyo.
Vailet mkazi wa Njiro Arusha alipigwa risasi na polisi katika jengo la Mamlaka ya Kodi ya Mapato (TRA) mkoani hapa, bado amelazwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi(ICU) katika Hospitali ya Kilutheri Arusha.
Mfanyabiashara huyo, aliyepigwa risasi Octoba 31, anadaiwa alitaka kumpiga risasi polisi aliyekuwa lindo kwa kutumia bastola yake baada ya kutokea sintofahamu ya maegesho ya magari.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Paul Kisanga alisema, hali ya mfanyabiashara huyo inaendelea vizuri.
Awali Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas alisema, mfanyabiashara huyo alipigwa risasi baada ya kulazimisha kuegesha gari hilo, mbele ya lango kuu la kuingia katika Tawi la Benki ya CRDB.
“Baada ya kutoka benki alikuta gari lake limetolewa upepo ndipo aliwafuata polisi waliokuwa jirani na lango hilo na kuanza kusemeshana nao hadi akapigwa risasi baada ya kutoa bastola yake.”