Kauli ya Mwisho ya Babu Seya na Papii Kocha kabla ya kurudishwa Gerezani



Ni dhahiri kwamba huu ndio mwisho wa harakati za Mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi Tanzania mwenye asili ya Congo DRC Nguza Viking na mtoto wake Johnson Nguza (Papii kocha) kujinasua kwenye kifungo cha maisha gerezani.

Kwa mara nyingine tena harakati zao za kujitoa kwenye adhabu hiyo zimegonga mwamba baada ya Mahakama ya Rufani kupigia msumari wa mwisho uliozima harakati zao kujinasua baada ya kutupilia mbali maombi yao ya marejeo ya hukumu ya rufaa yake.

hii ni mara ya tatu kwa wafungwa hawa kugonga mwamba baada ya Mahakama kuu kanda ya Dar es salaam na Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa zao kupinga hukumu ya Mahakama ya hakimu mkazi  kisutu iliyowahukumu kifungo cha maisha.

Wafungwa hawa kupitia kwa Wakili Mabere Marando walikua wakiiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya hukumu yake ya February 11 2010 iliyothibitisha adhabu hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya chini na badala yake iwaachie huru lakini Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa na Majaji watatu, Nathalia Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk ilitupilia mbali maombi hayo hivyo waendelee kutumikia kifungo cha maisha gerezani.

Ni uamuzi ambao uliibua machungu sio tu kwa Wafungwa na ndugu zao lakini hata kwa Wakili wao mwingine Gabriel Mnyele aliesema ‘hakuna namna nyingine ya kuwachomoa kwenye adhabu hii isipokua miujiza’
Ndugu na watu wengine waliohudhuria Mahakamani waliendelea kutokwa na machozi ya huzuni pale Wafungwa hawa walipokua wakipandishwa kwenye gari la Magereza kurudishwa kuendelea kutumikia adhabu yao.

Kauli ya Mahakama baada ya kutupilia mbali maombi yao ni ‘Waomba Marejeo hao hawakuwa na hoja ya msingi kwa sababu hoja zilizotolewa sio tu hazikidhi kuifanya Mahakama irejee hukumu hiyo bali pia zilishatolewa wakati wa usikilizwaji wa rufaa na kutolewa uamuzi na kwamba waomba Marejeo hawakuweza kubainisha makosa waliyodai yalijitokeza kwenye hukumu iliyowatia hatiani na hawakuweza kueleza ni jinsi gani yalisababisha haki kutotendeka’

Mahakama hiyo imesema ‘kuhusu upande wa mashtaka kushindwa kuwaita Mahakamani mashahidi wanaoonekana kuwa muhimu kuunga mkono ushahidi wa Watoto, tunasema hoja hiyo haina msingi…. suala la shahidi gani aitwe Mahakamani kuthibitisha kesi ya upande wa mashtaka liko mikononi mwa upande wa mashtaka, zaidi ya yote idadi ya Mashahidi sio hoja ya msingi bali kuaminika kwao’
Wakili Mnyele amesema ‘huu ndio mwisho wa mchakato, kulinganisha na hukumu ilivyokua ni kwamba kunahitajika kuwepo na Mahakama ya juu zaidi ya hii, kungekuwepo na Supreme Court ingeweza kusikiliza na kufikia maamuzi ya haki’

Kwa upande wake, Babu Seya wakati akipelekwa na askari kwenye gari la Magereza alitoa kauli ambayo hakuipa ufafanuzi wowote baada ya kuisema kwamba ‘kwa binadamu ni makosa lakini kwa Mungu hakuna makosa’

Papii Kocha nae wakati anapelekwa kupanda gari arudishwe Magereza alisema ‘sasa tunamuachia tu Rais ndie anaweza kutoa uamuzi wa mwisho’

Babu Seya na wanawe watatu walihukumiwa adhabu ya maisha gerezani na Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu June 25 2004 baada ya kupatikana na hatia ya kuwabaka na kuwalawiti watoto kumi wa kike wenye umri chini ya miaka 10.

Join Swahili One Community, "Like" and you will be one of us forever

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
Copyright © 2013. swahili one Blog - All Rights Reserved
Customized by: Grace Tommy The One | Powered by: BS
Designed by: Creative Blogger