MKE AISHI NA WANAUME WAWILI NDANI YA CHUMBA KIMOJA



DUNIA ina kila kituko, kama hujawahi kukisikia omba Mungu akupe uzima!  Mama mmoja, aitwae  Elizabeth Selestine, mkazi wa Kigogo-Mburahati, Dar hivi karibuni alizua timbwili nyumbani kwake baada ya majirani, wajumbe na ndugu zake kumjia juu kwa kitendo chake cha kuishi na wanaume wawili kwenye chumba kimoja, Ijumaa lina mkasa kamili.

Ndani ya timbwili hilo, watu kibao walikuwepo, lakini muhimu sana ni mdogo wa mwanamke huyo, Oscar Selestine (17) ambaye alianika kila kitu.
Oscar alisema shemejiye anaitwa Benedicto Ludovic na dada yake huyo walipanga kwenye nyumba ya akina Juma Ngulumo ambaye ndiye mwanaume wa pili, yaani hawara.

“Baada ya kuanzisha uhusiano na Juma, mwenye nyumba (baba wa Juma) aliwafukuza akiogopa kuwa kwa tabia ya dada lisije likatokea balaa kubwa. Hata mimi na mdogo wangu tuliishi kwa dada na shemeji.
“Dada na shemeji  wakahamia kwenye chumba kimoja nyumba ya jirani, dada akaniambia mimi na mdogo wangu mwingine tuishi nao huku tukitafuta pa kulala kwa sababu wao walipata chumba kimoja ambacho tulikuwa tunalala wote, mimi, mdogo wangu, dada, shemeji na watoto wao wawili.

“Lakini siku moja nilishangaa kumwona Juma akija na godoro hapo hapo kwenye chumba kimoja huku shemeji akiwemo,” alisema Oscar na kuwashangaza hata mapaparazi. Dunia ina mambo mengi.
“Nilishtuka sana! Kulala kwenyewe, shemeji  na dada kitandani, Juma akawa analala chini wakati na yeye ni mtu mzima tena ana watoto,” alisema Oscar.

Oscar aliendelea kusema kuwa, siku moja alishangaa kumwona Juma akimpiga dada yake, alipojaribu kuuliza dada huyo  akamjibu: “We mtoto, hayakuhusu.” Mwisho yeye na mdogo wake wakafukuzwa na kuambiwa wasifike  nyumbani hapo.
Oscar hakuona sababu ya kufunga kinywa bila kumalizia kusema yote, akaanika kwamba ilifika mahali Juma alianza kumpiga shemeji yao kisa eti amekuwa na wivu kwa mke wake. Makubwa hayo!

“Kumbe mtoto mmoja wa dada alikuwa akiona kila kitu, siku moja akaanika siri kwamba, Juma huwa anampiga shemeji usiku na ili amuache dada alale naye chini,” alisema Oscar.
Oscar akasema hakuna siri ya watu wawili, baadaye habari zilizagaa kwa ndugu wote kuwa dada yao anaishi na wanaume wawili, ndipo mama mwenye nyumba alimuita na kumkanya lakini hakusikia.

Mwenye nyumba alipoona jeuri hiyo alimuita tena na kumpa siku saba aondoke ndani ya nyumba yake lakini bado Elizabeth hakufanya hivyo.
Oscar tena: “Huwezi amini ilifika wakati shemeji akileta chakula kinapikwa halafu yeye hatengewi, anatengewa Juma, shemeji akiuliza anaambiwa akale na watoto. Sisi hatumuelewi shemeji, kama ni madawa basi yamemkolea sana.”

Ikadokezwa kwamba tukio hilo lilifika mbali, hadi kwa  wazazi wa mwanaume, Kilosa, Morogoro ambao walifunga safari mpaka Dar lengo lilikuwa kuwachukua wajukuu na mtoto wao Benedicto, lakini ilishindikana kwani waliambulia kutukanwa na mwanamke huyo, wakaondoka wakiacha laana nyuma.

Vituko viliendelea siku hadi siku, siku moja Benedicto au maarufu kwa jina la ‘baba Gire’ alikwenda kwa mjumbe wa eneo hilo, Maua Thabiti  huku akilia na kuapa ipo siku atafanya kitu kibaya ambacho mkewe na Juma hawatakaa wakisahau.
Mjumbe huyo ambaye ni wa shina namba 48, mtaa wa National Housing Mburahati, Dar alikiri kupokea malalamiko hayo lakini akasema mwanaume huyo anaogopa kuweka wazi kwa sababu atapigwa, hivyo anamuachia Mungu.

Mwenye nyumba wanayoishi watu hao, Flora Mtumbati alipoulizwa naye alikiri kuwa, Eliza anaishi na wanaume wawili.
“Baada ya kubaini hilo, Eliza aliitwa na Jumuiya ya Katoliki anakosali na kuonywa. Mimi nilimpa siku saba za kumtoa Juma na kubaki na mumewe, aliniahidi lakini hakufanya hivyo, bora watu wa magazeti mmekuja mnaweza kunisaidia,” alisema Flora.
Baada ya kuongea na vyanzo vyote, gazeti lilimtafuta Elizabeth:

“Huyu bwana (Juma) alikuja kwangu kwa matatizo, alikaribishwa na mume wangu, nilimkaribisha chumbani kwangu kwa sababu ndiyo chumba hichohicho. Hata hivyo, leo (Ijumaa iliyopita) anahama.”
Baada ya waandishi kuondoka, mwanamke huyo alitishia kujiua. Siku ya pili, waandishi waliambiwa kuwa mwanamke huyo alikimbilia Kimara  kwa wifi yake ambaye ni ndugu wa Juma.

Benedicto alipopatikana alisema: “Sikuamini kama mke wangu anatembea na Juma ingawa niliwahi kusikia. Kuhusu kupigwa ni kweli hasa akilewa pombe. Baada ya sakata hili mke wangu amesema kwa watu kuwa hata mtoto wa mwisho si wangu, ni wa Juma. Inauma sana.”

Baada ya waandishi kuibua ishu na watu kujaa, inadaiwa  Juma alitafuta vijana na kumpa kichapo cha nguvu baba Gire ambapo ameshonwa nyuzi kumi na mbili mdomoni na jichoni.
Kesi hii ilifikishwa Kituo cha Polisi Mburahati na kufunguliwa jalada namba MBR/RB/1204/13  KUJERUHI.

Join Swahili One Community, "Like" and you will be one of us forever

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
Copyright © 2013. swahili one Blog - All Rights Reserved
Customized by: Grace Tommy The One | Powered by: BS
Designed by: Creative Blogger