Wakenya wamtaka Uhuru ahudhurie ICC


Idadi kubwa ya Wakenya wanataka Rais Uhuru Kenyatta kuhudhuria vikao vya kusikilizwa kwa kesi dhidi yake katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) mjini Hague.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Utafiti la Ipsos Synovate unaonyesha kuwa asilimia 67 ya Wakenya waliohojiwa wanataka Rais Kenyatta kuhudhuria vikao vya kusikilizwa kwa kesi dhidi yake huku asilimia 25 wakitaka akatae kwenda katika mahakama hiyo ya ICC.
Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa juzi jijini Nairobi yanaonyesha kwamba asilimia 42 ya Wakenya wanataka kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta , makamu wa Rais William Ruto na aliyekuwa mtangazaji wa Redio Joshua Arap Sang ziendeshwe katika mahakama ya ICC. Asilimia 30 wanataka kesi dhidi ya Wakenya hao watatu ziondolewe kabisa huku asilimia 13 wakitaka kesi hizo zisikilizwe nchini humo.
Wengine asilimia 9 wanataka kesi ziendeshwe katika mahakama ya ICC bila washtakiwa kuwepo binafsi mahakamani hapo na ni asilimia mbili pekee ya Wakenya wanaotaka kesi hizo kuahirishwa kwa muda wa mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa kati ya Septemba 1 na 9, mwaka huu, ni asilimia 17 na 25 pekee ya wakazi wa mikoa ya Kati na Rift Valley mtawalia wanaotaka kesi ziendelee jinsi ilivyo katika mahakama ya ICC; ikilinganishwa na asilimia 75 na 63 ya wakazi wa Nyanza na Pwani mtawalia.
“Wanaotaka kesi hizo kuendeshwa katika mahakama ya ICC walisema kuwa ni katika mahakama hiyo pekee ambapo waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 watapata haki yao. Pia wanasema kuwa bado hawana imani na mahakama ya humu nchini ,” alisema Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa wa Ipsos Synovate Dk Tom Wolf, Shaka.
Alisema wanaotaka kutupiliwa mbali kwa kesi hizo walisema kuwa ushahidi dhidi ya Wakenya hao watatu ni wa kutiliwa shaka hivyo kuendelea na kesi hizo huenda kukasababisha uhasama zaidi.
Mwananchi.

Join Swahili One Community, "Like" and you will be one of us forever

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
Copyright © 2013. swahili one Blog - All Rights Reserved
Customized by: Grace Tommy The One | Powered by: BS
Designed by: Creative Blogger