Zitto Anusurika Kuuawa zaidi ya Mara Saba



MEDANI ya siasa imezingirwa na wingu la Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kuvuliwa nyadhifa zote za uongozi huku akitakiwa kujieleza ndani ya siku 14 ni kwa nini asivuliwe uanachama.
Zitto Kabwe akiongea na wanahabari juzi.
Huku kila jicho likijikita huko, kaka mkubwa wa Zitto, Salum Mohamed, alisema kuwa kama familia wamekuwa wakipata wakati mgumu sana kuhakikisha wanalinda usalama wa ndugu yao huyo, kwa sababu amekuwa akiwindwa kwa kila namna.
“Tunaongeza ulinzi, tunahakikisha watu wabaya hawamkaribii. Hatuamini watu ovyoovyo,” alisema Salum na kuongeza:
“Kwa kifupi matukio ya Zitto kunusurika kuuawa ni mengi lakini kwa haraka naweza kukumbuka saba.”
ACHAMBUA MATUKIO
Salum alisema, tukio la kwanza ni mwaka 2007, analielezea: “Zitto alipewa maziwa yenye sumu kwenye hoteli moja pale katikati ya Jiji la Mwanza. Marehemu Amina Chifupa alishtukia, akampigia simu akamtaarifu asinywe. Zitto alikuwa ameshakunywa na muda mfupi baadaye alipoteza fahamu. Alikimbizwa Hospitali ya Bugando ambako alitibiwa.
“Lipo tukio la Morogoro, alikuwa anatokea kwenye mkutano wa Chadema, kuna wapuuzi walilegeza nati za matairi ya gari ili apaje ajali njiani. Dereva alishtuka gari likiyumba kabla halijaanza kuchanganya mwendo, alipoliangalia, alikuta nati zimelegezwa.
“Kuna sakata la kumvamia mama yetu (Shida Salum), lile pia wahusika walimlenga Zitto na lengo lao lilikuwa kumuua. Mwaka 2011, kuna SMS ilibambwa ikiwa inaeleza mbinu za kumuua Zitto.
“Vilevile yupo dereva wa lori la simenti aliyemfuata Zitto na kumpasulia ukweli kwamba yeye alipewa kazi ya kumgonga kwa gari lake na kumuua lakini hawezi kufanya kwa sababu anamkubali sana.”
Salum aliongeza: “Yapo matukio mengine mawili ambayo kwa hakika yalikuwa ni mpango wa kumuua Zitto, kwani mazingira yanaonesha hivyo na hata sisi familia tunaamini hivyo.”
Mama mzazi wa Zitto, Shida Salum.
BI MKUBWA ASEMA
Upande mwingine, mama mzazi wa Zitto, Shida Salum alisema: “Maisha ya mwanangu yapo shakani, kuna wakati nikisikia hodi moyo unapiga pah! Maana nahisi pengine watu wanaomtafuta Zitto ndiyo wamefika.”
ZITTO AITEGA KAMATI KUU
Upande mwingine, Zitto (pichani kushoto) katika mkutano wake na waandishi wa habari Jumapili iliyopita jijini Dar, alisema: “Sing’oki Chadema na hakuna mtu wa kuniondoa kwenye chama hiki.”
Kauli hiyo ni kama kuitega Kamati Kuu ya Chadema ambayo imempa siku 14 ajieleze ni kwa nini asifukuzwe uanachama.

GPL

Join Swahili One Community, "Like" and you will be one of us forever

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
Copyright © 2013. swahili one Blog - All Rights Reserved
Customized by: Grace Tommy The One | Powered by: BS
Designed by: Creative Blogger