USHIRIKINA WATAJWA KIFO CHA MTOTO MGONJWA WA MGUU
KIFO cha ghafla cha mtoto Suleiman Rajabu (17) aliyekuwa na tatizo la mguu mmoja kuvimba tangu utoto kilichotokea Desemba 6, 2013 nyumbani kwao, Kitunda-Kivule ‘Bombambili’, Dar kimeibua mengi, lakini zito ni ushirikina kuhusishwa, Uwazi limeambiwa.
Suleiman ilikuwa apelekwe India kwa matibabu, Desemba 8, 2013. Maandalizi yote ya safari yalishakamilika.
Baadhi ya ndugu waliozungumza na Uwazi msibani hapo, walitoa sauti zao wakituhumu kuwa kuna mkono wa mtu katika kifo hicho kutokana na mazingira yake.
Ndugu mmoja ndani ya wanafamilia ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kilichomsukuma kunena hayo kwa ujasiri ni kuona kwamba mtoto huyo alizaliwa na tatizo hilo, sasa ana miaka 17 na katika muda wote familia ilihangaika kutafuta tiba, “iweje leo, siku moja kabla ya kusafirishwa kwenda India kwa matibabu ndiyo afariki dunia?
“Kufa kupo lakini kwa Suleiman aliyeishi kwa mateso kwa miaka kumi na saba mpaka juzijuzi tu Kampuni ya Global Publishers ikaandika habari zake na watu wakamsaidia mtoto, iweje afe siku moja tu kabla ya safari?” alihoji ndugu huyo.
Waombolezaji wengi waliokutwa msibani hapo pia nao walizungumzia uwezekano wa ushirikina kuhusishwa.”
Habari za ugonjwa wa mtoto huyo zilikuwa zikiandikwa na Magazeti Pendwa ya Global Publishers ambapo picha yake pia ilionesha jinsi mguu mmoja ulivyovimba kimaajabu na kumfanya ashindwe kutembea maishani mwake.
Familia yake iliomba msaada kwa wasamaria wema ili mtoto huyo atibiwe. Awali baada ya kupata kiasi cha fedha, alipelekwa Hospitali ya CCBRT ya jijini Dar ambako walishauri apelekwe India.
Mmoja wa watu walioguswa na kumlilia mtoto huyo kabla na baada ya kifo ni mtangazaji wa televisheni wa kituo cha Channel Ten ambaye pia ni Miss Tanzania 1999, Hoyce Temu ambaye pamoja na masikitiko yake alianzisha utaratibu wa kutafuta njia za kumsaidia mgonjwa huyo kupitia kipindi chake cha Mimi na Tanzania kinachorushwa hewani na Runinga hiyo na kutoa misaada mbalimbali ya hali na mali.
Kupitia kipindi hicho na magazeti ya Global, michango iliyokusanywa ili kumsaidia ilifikia shilingi milioni 13 ambapo sehemu ya fedha hizo zilishalipwa kwenye Hospitali ya Ganga, India ambako marehemu ilikuwa apelekwe kwa matibabu Jumapili iliyopita.
Mratibu wa safari iliyokufa ya Suleiman, Imelda Mtema ambaye ni mwandishi wa habari wa Global Publishers alisema juzi kuwa, kwa vile fedha za kumlipia marehemu zilishalipwa India na haziwezi kurudishwa, mtoto Hamis Hashim ambaye naye ana tatizo kama la marehemu Suleiman atapelekwa nchini humo kutibiwa.
Baba mzazi wa Suleiman, Rajabu Upinde aliwashukuru wote walioguswa na mwanaye hasa walioendesha harakati za kufanikisha michango ya mtoto huyo lakini akasema haikuwa riziki.
Mazishi ya Suleiman Rajabu yalifanyika Desemba 7, mwaka huu Mwaneromango, wilayani Kisarawe mkoani Pwani. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.