Yanga Yampa Matumaini Barthez
Licha ya kufanikisha usajili wa kipa mkongwe, Juma Kaseja, uongozi wa Yanga umesema hauna mpango wa kumtoa kwa mkopo kipa wake aliyetetereka, Ali Mustafa ‘Barthez’.
Wiki iliyopita Yanga ilitangaza kumsajili Kaseja kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 40 milioni na kuifanya timu hiyo iwe na jumla ya makipa watatu, kwani tayari ilikuwa na Barthez na Deogratius Munishi ‘Dida’.
Hata hivyo, usajili wa Kaseja ndani ya kikosi cha Yanga ulitafsiriwa na baadhi ya mashabiki wa soka kuwa ndiyo mwanzo wa kuondolewa kwa Barthez ambaye alipoteza nafasi ya kuwa kipa namba moja tangu alipotunguliwa mabao matatu katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya Simba lililomalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Hata hivyo, jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdalah Bin Kleb alisema, Barthez ataendelea kuwamo kwenye kikosi cha timu yake sambamba na Kaseja na Dida.
“Mwalimu wetu (Ernest Brandts) aliacha mapendekezo ya wachezaji anaowataka wasajiliwe na usajili wa Kaseja ni sehemu ya kutekeleza mapendekezo hayo.
“Tunataka tuwe na makipa watatu wa uhakika ndiyo maana tumemwongeza Kaseja, lakini hatuna mpango wa kumtoa kwa mkopo kipa yeyote si Barthez wala Dida,” alisema Binkleb na kuongeza:
“Makipa watatu si wengi na hata kama mwalimu atasema anataka mwingine tena sisi tutatekeleza. Kama unavyojua michuano ya Ligi ya Mabingwa si lelemama unatakiwa ujiimarishe sawasawa.”
Katika hatua nyingine makipa Dida na Barthez wamesema wanamkaribisha kwa mikono miwili Kaseja na kuahidi kushirikiana naye kwa roho safi.
Wakizungumza kwa wakati tofauti, Dida na Barthez wameliambia gazeti hili kuwa kwa upande wao hawana kinyongo na Kaseja isipokuwa wamefurahishwa na ujio wake Yanga.
“Hilo ni jambo la furaha kwetu kwa kukutana tena pamoja na hivyo ndivyo maisha ya soka yanavyokuwa. Hakika hatuna budi kwa pamoja kushukuru Mungu kwa kutukutanisha tena.
“Kazi yangu ni kujituma uwanjani kila ninapopata nafasi naamini na wenzangu pia watakuwa wakifanya hivyo,” alisema Dida ambaye amejiunga na Yanga msimu huu akitokea Azam.
Hata hivyo kwa upande wake Barthez alisema kuwa, ”Mimi na Kaseja ni marafiki na siyo maadui kama watu wanavyozusha na hilo litajulikana pindi tutakaporudi kutoka mapumziko.
“Nimeishi naye Simba kwa amani bila ya tatizo lolote akiwa kama nahodha wangu, kama tulipishana ni hali ya kawaida kwa binadamu. Namkaribisha Yanga na nitafanya naye kazi kwa roho safi bila ya tatizo lolote kama ilivyokuwa hapo awali.
“Kuhusu nafasi ya kucheza, kocha ndiye mwenye uamuzi nani acheze na nani asicheze, lakini nitaendelea kujituma mazoezini kama ilivyokuwa hapo awali,” alisema Barthez.