Showing posts with label Habari za Kitaifa. Show all posts

RAIA WAWILI NA POLISI WAWILI WAFARIKI KATIKA MAPIGANO HUKO MOROGORO


Watu watatu, akiwamo askari polisi wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kuzuka mapambano kati ya polisi na raia katika Kijiji cha Igwati, Tarafa ya Malinyi Wilaya ya Ulanga, Morogoro.
Diwani wa Kata ya Malinyi, Said Kila aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Leon Chikwita, Andrew Likomoka na Edson Kidunda.
Alisema mmoja wa majeruhi Idelfonce Malenga (35), hali yake ni mbaya baada ya kupigwa risasi shavuni. Majeruhi wawili majina yao hayakufahamika mara moja.
Diwani Kila alisema mauaji hayo yalitokea baada ya kundi la wakulima kuvamia Kituo cha Polisi Malinyi kushinikiza kuachiwa kwa wenzao watatu waliokuwa wanashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mfugaji mmoja wa kijiji hicho hivi karibuni.
“Baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwa wenzao walifika kituo cha polisi ambako, hawakuwakuta watuhumiwa hao kwani walikuwa wamehamishiwa kituo kingine,” alisema diwani huyo.
Alisema katika jitihada za kulinda kituo, polisi walitoa tahadhari mbalimbali za kuwataka wananchi hao kutawanyika ikiwamo kupiga mabomu ya machozi, lakini waliendelea kukaidi amri hiyo na badala yake walizidi kujikusanya na kukivamia na kisha kukichoma moto pamoja na gari la askari lililokuwapo. Katika shambulizi hilo, ndipo mauaji hayo yalipotokea.
Chagonja eneo la tukio
Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema ametuma timu maalumu ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja kwenda kuongeza nguvu katika operesheni ya kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso ilisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, IGP Mwema ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususan, Kata ya Malinyi kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi wakati uchunguzi ukiendelea.
Chanzo cha mgogoro
Mgogoro kati ya wafugaji na wakulima wa Igwati ulianza Desemba 13, mwaka huu wakati kundi la wananchi lilipomkamata mfugaji huyo na kumpeleka katika ofisi za kijiji.
Ilidaiwa kuwa baada ya kumfikisha, mtendaji wa kijiji alimfungia mtuhumiwa huyo ofisini kwake na kuanza kuhoji sababu za wananchi kumkamata jambo ambalo linaelezwa kwamba liliwakera na kuanza kumshambulia hadi kuikimbia ofisi na kumwacha mfugaji huyo ambaye alishambuliwa na kuuawa.
Kitendo cha kukamatwa na kupigwa hadi kuuawa kwa mfugaji huyo kinadaiwa kuwa kilikuwa cha kulipiza kisasi baada ya wafugaji kuvamia nyumbani kwa Mjumbe wa Kamati ya Mazingira, Victoria Marietha na kumjeruhi vibaya kisha kufariki dunia katika Hospitali ya Lugala, Malinyi alikokuwa akipatiwa matibabu.

Read More »

AFANDE AACHA LINDO BENKI NA KWENDA KUMKAMATA DEREVA WA BODABODA


Afande akiwa amemdhibiti dereva wa bodaboda.
Wasamaria wema wakijaribu kumbembeleza afande.
Afande akiwa…
Afande akiwa amemdhibiti dereva wa bodaboda.
Wasamaria wema wakijaribu kumbembeleza afande.
Afande akiwa amecharuka hataki kusikia cha mtu.
Afande kakomaa.



Afande aliyekuwa akilinda Benki ya NMB iliyopo Mtaa wa Samora karibu na Idara ya Habari 'Maelezo' jijini Dar, leo mchana aliacha lindo lake na kuanza kukamata bodaboda zilizokuwa zikivunja sheria za usalama barabarani kama anavyoonekana pichani akimdhibiti mwendesha bodaboda.

Read More »

ABIRIA 213 WANUSURIKA KIFO BAADA YA NDEGE YAO KUTUA KWA DHARULA KATIKA UWANJA MDOGO WA ARUSHA


Abiria 213 waliokuwa wakisafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia jana walinusurika kifo baada ya ndege hiyo kutua kwa dharura katika uwanja mdogo wa Arusha.
Ndege hiyo aina ya Boeing 767, ilitua saa 6.45 mchana katika uwanja huo baada ya kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kutokana na kupata pancha kwa ndege nyingine inayomilikiwa Shirika la Ndege la Tanganyika (TFC), kwenye njia ya uwanja huo.

Ndege ya Ethiopia ililazimika kuelekea Arusha na kutua kwenye uwanja huo mdogo kuweza kupokea ndege kubwa kutokana na kuishiwa mafuta.
Ndege hiyo iliyokuwa inatokea Addis Ababa, Ethiopia ikiwa pia na wahudumu 23, baada ya kutua kwenye Uwanja wa Arusha, ilinasa kwenye tope baada ya tairi lake la mbele kuvuka sehemu ambayo lami inaishia kutokana na ufupi wa njia zinazotumiwa na ndege zinapotua kwenye uwanja huo.
Jitihada za kuiondoa ndege hiyo zilishindikana jana. Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Johannesburg, Afrika Kusini kwa kupitia Kia na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema: “Rubani amejitahidi kutua katika uwanja huu japo ni mdogo ili kuokoa maisha ya abiria kwani walikuwa hawana mafuta ya kutosha kwenda uwanja mwingine.”
Tukio la ndege hiyo kutua kwa dharura limekuja siku chache tangu ndege ya Shirika la Ndege la Precision iliyokuwa na abiria 37 kupasuka matairi manne ilipokuwa ikitua kwenye Uwanja wa KIA Jumamosi 


Read More »

CHADEMA WAZIDI KUMKAA KOONI ZITTO


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakitashughulikia rufaa iliyokatwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwa Baraza Kuu kupinga uamuzi wa Kamati Kuu (CC) wa kumvua nyadhifa zake katika chama, hadi hapo itakapopitia utetezi wake na kuamua hatima ya uanachama wake katika chama hicho.
Pia kimethibitisha kupokea utetezi dhidi ya mashitaka 11 yanayohusisha usaliti dhidi ya chama na kuwachafua viongozi wakuu kupitia waraka wa mabadiliko.
Mashtaka hayo yanamkabili Zitto, pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa CC, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Victor Kimesera, alisema hayo alipozungumza na NIPASHE, ofisini kwake, jijini Dar es Salaam jana.
Kimesera, ambaye ni Katibu Mtendaji Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema, alisema rufaa hiyo ni kitu kidogo, hivyo haiwezi kuanza kushughulikiwa na chama katika sakata la Zitto na watuhumiwa wenzake.
“Kuna (kitu) kikubwa cha mbele yake (rufaa),” alisema Kimesera akijibu swali la NIPASHE lililotaka kujua nini kinaendelea kwenye chama baada ya Zitto kukata rufaa.
 Kimesera alisema kitu kikubwa kuliko rufaa, ambacho kitaanza kushughulikiwa na chama ni maelezo ya utetezi wa Zitto na watuhumiwa wenzake.

Alisema hiyo ni kwa sababu tayari kuna hoja ya CC, ambayo inataka ijiridhishe kama Zitto na wenzake waendelee kuwa uanachama au la.

 Kwa mujibu wa Kimesera, baada ya Zitto na wenzake kuwasilisha utetezi wao, CC itaitishwa na kuyapitia na kisha itatoa maamuzi juu ya uanachama wao.
“Sasa huwezi kuongea juu ya rufaa wakati hujajua uanachama wao kwanza,” alisema Kimesera.

 Hivyo, alisema rufaa ya Zitto itaendelea kuhifadhiwa kwenye jalada hadi hapo hatua ya kwanza ya kupitia maelezo yao ya utetezi na kuyatolea maamuzi itakapochukuliwa. “Lazima twende kwa hatua. Kwa hiyo, hiyo (rufaa) imekaa,” alisema Kimesera.

 Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando, alitaja sababu mbili za mteja wake kukata rufaa kuwa ni kukiukwa kwa taratibu za kuchukua hatua za nidhamu na sababu zilizotolewa kutokuwa sahihi.

Msando alitaja kifungu cha 6.5.6 cha Kanuni ya Uendeshaji ya chama hicho, akisema utaratibu uliotakiwa kufuatwa kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni ni kupewa kwanza mashtaka kwa maandishi ili apate nafasi ya kujibu.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
 Alisema kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu bila kwanza kupewa mashtaka yake kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kujibu mashtaka kwa maandishi.

Alitaja  ibara ya 5.4.3 na 5.4.4 ya Katiba kwamba mwanachama yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.”

 Alitaja vipengele vingine ni kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika na atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao ndani ya wiki mbili baada ya kusikilizwa.

 Katika hatua nyingine, Kimesera alisema Chadema imepeleka majibu baada ya Mwigamba kupeleka barua yenye malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa dhidi ya uongozi wa chama hicho.

Katika malalamiko yake, Mwigamba anadai kuwa katiba ya Chadema ilivurugwa na viongozi wa chama kwa kuondoa kinyume cha taratibu maelezo ya kifungu cha katiba ya chama yaliyokuwa yakiainisha ukomo wa vipindi viwili vya uongozi.

 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, alithibitisha kupokea barua hiyo ya Mwigamba na kusema ofisi yake inaifanyia kazi.

 Kimesera jana aliliambia NIPASHE kuwa walipeleka majibu dhidi ya malalamiko ya Mwigamba baada ya kuagizwa na msajili kufanya hivyo kabla ya Desemba 19, mwaka huu.

 Katika barua yake, Mwigamba amemuomba msajili kutoa mwongozo kuhusu anachodai kuwa ni mgogoro wa kikatiba uliopo ndani ya Chadema kufuatia kipengele cha katiba kinachogusia ukomo wa uongozi kubadilishwa kinyume cha utaratibu.

 Novemba 22, mwaka huu, CC iliwavua madaraka viongozi hao na kuwataka wajieleze kwa maandishi ndani ya siku 14 baada ya kudaiwa kuhujumu chama kwa kuandika waraka wa siri unaodaiwa pamoja na mambo mengine, kuwadhalilisha viongozi wakuu wa Chadema.
 



CHANZO: NIPASHE

Read More »

BINTI WA MIAKA 17 ANASWA AKIJIUZA KATIKA GESTI BUBU


KIKOSI kazi cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ Kanda ya Ziwa, kinaendelea kufukua uchafu unaofanyika jijini hapa, safari hii kimemnasa binti mwenye umri chini ya miaka 18 akifanya ukahaba wikiendi iliyopita bila wasiwasi wowote.
Anitha baada ya kunasa katika mtego wa OFM.
OFM Kanda ya Ziwa, kikiwa ni kitengo kipya kilichoteuliwa rasmi kushughulikia kadhia za mikoa yote inayozunguka Ziwa Victoria kilinasa tukio hili laivu na kulifuatilia kwa kina ili kutoa ukweli kamili kwa jamii.
HABARI KAMILI
Timu yetu ilishuhudia binti huyo akiwa amechanganyikana na mabinti wengine wakubwa wakijiuza kwa wateja wa baa mbalimbali katika eneo la Mabatini jijini hapa huku wakitumia gesti bubu iliyopo maeneo hayo.
Kwa siku tatu mfululizo, mapapazari wetu walimfuatilia na kujionea namna binti huyo mdogo akichukuliwa na mababa watu wazima na kwenda kula nao uroda kwa nyakati tofauti.
Anitha akivaa nguo zake baada ya kunaswa akifanya ukahaba.
AINGIA MTEGONI
Ili kupata ushahidi wa tukio hilo, makamanda wetu waliingia mzigoni na mmoja wao akajifanya mteja ambapo alimtokea binti hiyo ambaye alikubali kwenda kulala naye  kwa dau la shilingi 5,000.
Binti huyo aliyejitambulisha kwa jina la Anitha aliongozana na kamanda wetu hadi ndani ya gesti bubu inayotumika kwa uchafu huo bila kujua kwamba alikuwa ameingia ‘choo cha kiume’.
Anitha akiohojiwa baada ya kunaswa akiwa kazini.
OFM KAZINI
OFM wakiwa na wadau wengine waliokubali kushiriki katika zoezi hilo ambalo ni aibu kwa uongozi wa jiji hili na serikali kwa jumla, walikuwa tayaritayari jirani na gesti  hiyo wakisubiri maelekezo kutoka kwa kamanda aliyeingia na changudoa huyo mtoto.
Vifaa vya mawasiliano vya OFM vilifanya kazi yake vyema ambapo kamanda aliyekuwa chumbani alitoa maelekezo kwa wenzake kuwa changudoa yule, alikuwa amesaula ndipo wakaingia na kufotoa picha za kutosha.
MSIKIE MWENYEWE
Alipogundua kuwa kumbe ulikuwa mtego wa kumnasa aliomba asamehewe kwa madai kwamba alilazimika kufanya vile kwa lengo la kujitafutia maisha kwa vile kwao hali ni mbaya.
Anitha akiwa mikononi mwa wanausalama.
“Jamani mimi ni mdogo, nina miaka 17, sina baba wala mama na hali ya maisha ni ngumu ndiyo maana niliamua kuingia kwenye biashara hii,” alisema Anitha.
Hata hivyo, uchunguzi wa Risasi Mchanganyiko, umeonyesha kuwa, Anitha ni muongo kwani ametoroka nyumbani kwao Mahina, Nyakato ambako alikuwa akiishi na wazazi wake na kukatisha masomo yake akiwa kidato cha pili.
Chumba alipokutwa Anitha kitandani pakiwa na kinga.



WAZAZI SOMENI HAPA
OFM inatoa wito kwa wazazi kuwa makini na malezi ya watoto wao kwa kuwafuatilia mara kwa mara ili wasiharibike na kuiga tabia kama ya Anitha. Aidha, wazazi wa Anitha wanapaswa kuchukua hatua za makusudi kumwondoa binti yao katika biashara hiyo mbaya inayohatarisha usalama wa afya yake.

Read More »

MAMA SHARO MILIONEA AMTOA MACHOZI ICH MAVOKO


STORI kuhusu maisha ya mama mzazi wa staa wa komedi Bongo, marehemu Husein Mkiety ‘Sharo Milionea’, baada ya kifo cha mwanaye huyo imemliza Rich Mavoko ambaye alikwenda kumtembelea nyumbani kwake kijijini Lusanga, Muheza mkoani Tanga.
Rich Mavoko akifuta machozi alipomtembelea Mama Sharo Milionea.
Akiteta machache na Risasi Vibes, Mavoko alisema, yeye kama msanii aliguswa kwenda kumsalimia mama Sharo kwa kuwa wote ni wasanii na aliona mama huyo anahitaji faraja kutoka kwa watu waliokuwa karibu na mwanaye.
“Mama alifurahi sana kuniona. Tulizungumza mengi lakini niliguswa sana na matatizo aliyonayo mama yetu. Mama anasema, mali nyingi za marehemu mwanaye, amekuwa akizisikia tu lakini hajapewa.
Mavoko na Mama Sharo wakiwa katika kaburi la Marehemu Sharo Milionea.
“Kiukweli mama Sharo anatia huruma sana kwani faraja imepotea, mali za mwanaye hazioni, amebaki akitia huruma.
Unajua marehemu alikuwa akimsadia sana mama yake, ndiyo lilikuwa tegemeo lake kubwa. Ameondoka na kumuacha akiwa hana la kufanya, mbaya zaidi hata mali zake ambazo zingepaswa kumsaidia kipindi hiki, wajanja wamezidhulumu.
“Dunia haina usawa kabisa. Kiukweli inatia huruma sana. Nawasihi wasanii wenzangu na wadau wa sanaa, inatakiwa tukumbuke wenzetu waliotangulia tena kwa kuwaenzi kwa kila njia.
Marehemu Sharo Milionea enzi za uhai wake.



Kuna vitu vinauma sana amenieleza tangu kifo cha mwanaye haki zake nyingi hajui zilipo. Tuungane wasanii tuwasaidie wazazi wa wasanii wanaotangulia mbele za haki,” alisema Mavoko.

Read More »

MZEE WA KANISA ALIFUNGA KANISA! HUKO MBEYA


WAUMINI wa Kanisa la Nyumba ya maombi (House of Prayer Shield of Faith Christian Fellowship) lililopo jijini Mbeya wamekosa sehemu ya kufanyia ibada baada ya Kanisa lao kufungwa na mzee wa Kanisa hilo, Laurence Malongo.
Kanisa lililofungwa.
Mchungaji wa Kanisa hilo, Owden Mwakifuna amesema hivi karibuni mzee Mwalongo alifika kanisani na kuwataka waumini wote kutoka huku akionekana kutawaliwa na jazba.
Mchungaji Mwakifuna alisema kanisa hilo lilijengwa baada ya Malongo kutoa uwanja kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo kama shukrani baada ya kufanyiwa maombi yeye na mwanawe na kupona magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua.
Viongozi wa kanisa wakiwa nje baada ya kanisa kufungwa.
Baada ya kanisa hilo kufungwa Mchungaji Mwakifuna alitoa taarifa kwa kiongozi wa kanda ya Mbeya, Mchungaji Isaya Laiser na kufanya vikao vya mara kwa mara ili kutatua mgogoro huo bila mafanikio.
Kufungwa kwa kanisa hilo lililopo kata ya Itezi kumewafanya waumini kutembea kilometa 10 hadi makao makuu ya kanda eneo la Pambogo Kata ya Iyela jijini Mbeya.
Ofisa Mtendaji wa Kata akihakiki viti.
Baada ya kufungwa kwa kanisa hilo, viongozi wa waumini hao waliandikia barua uongozi wa kata ambao uliitisha kikao Desemba 5 mwaka huu.
Kikao hicho chini ya Diwani wa Kata ya Itezi, Frank Mayemba ambaye alisema kiwanja hicho ni mali ya Malongo na hati yake haijabadilishwa.



Kikao kilimalizika kwa Malongo kuchukua viti 60 na kulifunga jengo hilo mbele ya uongozi wa kata ya Itezi na kuamriwa maandishi ya kanisa hili yafutwe kwenye kuta za jengo hilo mara moja.

Read More »

KIFO CHA KIGOGO WA CCM MWANZA, MAZITO YAIBULIWA


MAMBO mazito yameibuka baada ya kifo cha kigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Diwani wa Kata  ya Kisesa, Clement Mabina jijini Mwanza  kwa mwanasiasa mmoja kutajwa kuhusika na mauaji hayo, Risasi Mchanganyiko limeambiwa.
Clement Mabina enzi za uhai wake.
Habari zilizosambaa jijini hapa zinadai kwamba  mwanasiasa huyo (jina kapuni) andaiwa kuwagawia fedha baadhi ya wanakijiji waliohusika ili  kukatisha uhai wa Mabina.
“Hakuna asiyejua kwamba jambo hili lina mkono wa kisiasa ndani yake, mapema kabla ya marehemu kwenda Kanyama kwenye eneo la tukio mmoja wa wanasiasa mashuhuri alipita na kuwashawishi wanakijiji wasikubaliane na hoja zake na ikiwezekana wammalize,” alisema mmoja wa watu waliokuwa wakizungumzia kifo cha Mabina.
Mwili wa Mabina baada ya kushambuliwa.
Hata hivyo, polisi wanawashikilia watu saba wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo ya kinyama.
Kamanda wa Polisi wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACP, Valentino Mulowola, akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu, alisema hadi sasa watu saba wanashikiliwa na jeshi hilo.
Kamanda alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti jana ambapo jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika katika mauaji ya  diwani huyo ambaye zamani alikuwa ni mwenyekiti CCM Mkoa wa Mwanza.
Katika tukio hilo la mauaji, Mabina aliuawa kwa kukatwa mapanga na kupigwa mawe ambapo alikutwa na majereha makubwa kichwani sehemu za kisogoni.
Kabla ya kuawa na wananchi  hao, marehemu alimpiga risasi mtoto Temeli Malemi (11) kwa  bahati mbaya wakati akijihami na mashambulizi ya wananchi hao.
Imeelezwa na Kamanda wa Polisi SACP Mulowola kuwa marehemu alikutwa na silaha mbili aina ya Short-gun na bastola moja.
Hata hivyo ndugu wa marehemu walishindwa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kuhusiana na habari zilizoandikwa na mitandao ya kijamii kuhusisha kifo cha ndugu yao (Mabina) na masuala ya kisiasa.



Aidha habari kutoka eneo la tukio zainadai kuwa mmoja wa watuhumiwa alikamatwa na simu ya mkononi ya marehemu,hata hivyo kamanda hakutaka kutaja majina  ya watuhumiwa hao kuhofia kuvuruga upelelezi.

Read More »

RAGE ALIA NA WALIOMUUZA OKWI YANGA


MWENYEKITI aliyesimamishwa wa Simba, Ismail Rage, amefanya kikao na baadhi ya wanachama wa timu hiyo na kutoa siri kwamba waliomuuza mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa Yanga ni Waganda, SC Villa, lakini akasisitiza ni hujuma kutoka ndani ya klabu hiyo.
Emmanuel Okwi.
Championi Jumatano lilikuwa likipata ‘live’ kila kinachoendelea ndani ya kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya klabu ya Simba, barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam, jana.
Akionyesha mwenye masikitiko, Rage alisema kuna baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wanahusika katika usajili wa Okwi aliyetua Yanga kwa mkataba wa miaka miwili na nusu.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage.
Rage, amesema Okwi raia wa Uganda, mpaka sasa anakabiliwa na kesi tatu muhimu na kuzitaja ya kwanza ni ile ya nyota huyo kukakabiliwa na mashtaka ya kutoroka katika klabu yake ya zamani ya Etoile du Sahel ya Tunisia (ESS).
Shitaka la pili ni kuhusu SC Villa, ambao walipewa Okwi kwa mkopo lakini wakamuuza Yanga na tatu ni kesi yake aliyoifungua Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuhusu ESS, ambapo kabla ya shirikisho hilo kutoa majibu nyota huyo kukubali, Mganda huyo kauzwa Yanga.
“Nilipiga simu Fifa kutaka kujua kujua kuhusu Okwi, nikaambiwa kuna fedha dola 5,900 ambazo ni kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi yetu, mwisho ilikuwa saa nne asubuhi leo (jana). Barua ilishatumwa tangu Desemba 6, lakini hakuna aliyeijibu na wakaificha,” alisema Rage akitaka kudondosha chozi ‘live’.
“Saa tatu asubuhi nikatuma fedha hizo ambazo zitatoa nafasi ya kusikilizwa kwa jambo hilo. Kama ningechelewa, basi Okwi angeweza kuwa mchezaji huru kwenda Yanga,” alisema Rage katika kikao hicho kilichofanyika kuanzia saa 10:15 hadi saa 11:45 jioni.
Aidha, Rage amesema anajua kuwa kamati ya utendaji ya timu hiyo inachangia kumhujumu ili aonekane hafai katika klabu hiyo, ambapo sasa ataitisha mkutano mkuu Januari mwakani.
“Simba imejaa wanafiki, wanafanya mpango wachezaji waende Yanga. Mfano, Okwi alishatangaza anaitaka Simba, vipi hawakumsajili na utaona mambo yanaharibika kila nikiwa nje ya nchi. Pia TFF kuna watu kama hao na wanachangia kutuhujumu na kuniharibia,” alisema.
Kuhusiana na suala la uchaguzi, Rage rasmi ametangaza kwamba hatagombea nafasi hiyo tena na badala yake kuna mtu amemuandaa.
“Tayari nimemuandaa mtu, siwezi kumtaja sasa ila nitawaacha wanachama waamue utakapofika uchaguzi,” alisema Rage.
Mzigo wa Okwi umekuwa ukimuangukia Rage kwa kuwa ndiye alifunga safari kwenda kumuuza Tunisia, lakini akarejea mikono mitupu na dola 300,000 za mauzo zikabaki Tunisia na hadi leo ni hadithi.

    Read More »

    MKURYA HUYU AISHI NDANI YA HANDAKI KWA ZAIDI YA MIAKA MINNE HAPA DAR



    DUNIA haiishi vituko! Chacha Makenge (36)  mzaliwa wa Kijiji cha Kisangula, Mtukula, Serengeti mkoani Mara anaishi jijini Dar lakini ndani ya handaki aliloligeuza chumba kwa miaka minne sasa, ni ajabu lakini ni kweli.

    Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni nje ya handaki hilo lililopo mita chache kutoka majengo ya biashara ya Mlimani City, Makenge alisema alichukua uamuzi huo baada ya rafiki yake (jina linahifadhiwa) kumchomea nyumba na kuteketeza samani zote.

    “Ilikuwa mwaka 2009 mwanzoni rafiki yangu huyo ndiye alinipa sehemu ya kiwanja chake nijenge nyumba. Nikawa  naishi hapo huku nikiendelea na shughuli zangu za kila siku.

    “Siku moja akabadili mawazo, akanitaka nihame katika eneo lake bila kunipa sababu, nilimwomba anipe muda nitafute pa kwenda.

    “Julai 2009 akaja na polisi, akanikamata na kunipeleka Kituo cha Polisi cha Stakishari, nilipowauliza kosa langu, hawakunieleza.
    “Baada ya siku mbili majirani walikuja kuniona na kuniambia kwamba nyumba yangu imechomwa moto na kila kitu kilichokuwa ndani kimeteketea, aliyefanya hivyo ni rafiki yangu. Nilijisikia vibaya sana.

    “Siku iliyofuata majirani walikuja tena kituoni wakaniwekea dhamana. Nilipofika kwangu nilikuta majivu tu, iliniuma sana, nililia lakini sikupata ufumbuzi. Kwa vile nilikuwa sina pa kwenda ilibidi niwe nalala palepale nilipochomewa nyumba nikisaidiwa chakula na majirani.

    “Siku iliyofuata, saa nne usiku nilivamiwa na watu wanne, wakiwa na mapanga na marungu, nilipambana nao mpaka wakaondoka. Kesho yake nilikwenda kwa mwenyekiti wetu wa serikali ya mtaa, Jumanne Malima kumweleza yaliyonipata, alisikitika, akaniandikia barua kwenda Polisi Stakishari.

    “Nilipofika kituoni sikusikilizwa, badala yake walinikamata tena na kuniweka ndani wakidai kwamba nimefunguliwa kesi ya kumjeruhi mtu kwa panga. Hawakukubali niwekewe dhamana.

    “Julai 31, 2009 nilifikishwa Mahakama ya Mwanzo Ukonga na baadaye nilipelekwa Mahabusu ya Gereza la Keko, nikawa napelekwa mahakamani hadi Septemba mwaka huo ambako nilihukumiwa kwenda jela miezi 9.

    “Nilitumikia maisha ya jela hadi Desemba 10, 2009 nikatolewa kwa msamaha wa Rais Jakaya Kikwete. Nilikwenda kuishi kwa ndugu zangu huku wakifuatilia sababu ya kufanyiwa vitendo hivyo bila mafanikio.

    “Maisha ya kwa ndugu hayakunifurahisha kwani hata wao walikuwa na majukumu mengi, niliamua kuendelea na kazi zangu za sanaa pia utunzaji wa mazingira na bustani kwa watu wakawa wananilipa fedha.

    “Ndipo nilipoamua kutafuta sehemu iliyotulia ili niweze kuishi, nikapata hapa, ni jirani na Mlimani City. Nilichimba handaki kubwa kama unavyoliona, kwa chini kuna kitanda ninacholalia.

    “Kwa hakika hapa sipati shida, wala kelele. Kwanza ni tulivu sana, nimefikia hatua ya kuishi kama mnyama kutokana na mateso na bugudha nilizopata, wengi hawajui nilipo, nipo katika pori hili kwa miaka minne sasa,”alisema Makenge.

    GPL

    Read More »

    BILIONEA AKUTWA AMEFARIKI NDANI YA GARI DAR, ASEMEKANA KAJIUA MWENYEWE


    NI jambo lililotoa mshtuko kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani ambapo Desemba 10, mwaka huu, walikuta mwili wa binadamu ukiwa ndani ya gari lililopinduka, pembeni mwa Barabara ya Kisarawe - Mwaneromango.

    Mbali na mwili, ndani ya gari hilo aina ya Toyota RAV 4 (milango mitatu new model) lenye namba za usajili T 273 AKP kulikutwa bastola moja, risasi 85 na magazini mbili.

    Utata ukaanzia hapo, polisi wa wilaya hiyo wakiongozwa na mkuu wao (aliomba jina lisitiriwe kwa sababu si msemaji) wakajiuliza ni nani mtu huyo ambaye alikuwa amefariki dunia? Kumbe alikuwa Suleiman Muhema (42), bilionea kijana mkazi wa jijini Dar es Salaam.

    polisi waliuchukua mwili wake na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Wilaya mpaka ndugu walipokwenda kuuchukua kwa mazishi.

    SULEIMAN MUHEMA NI NANI?
    Suleiman Muhema ni mkazi wa jijini Dar, amejenga jumba la kifahari Kijitonyama ambako aliishi na mke wake, Zihji Mvungi (42).

    Mpaka kifo chake alikuwa mfanyabiashara wa magari kutoka Japan akiyauza Dar, pia alikuwa na kampuni ya usafirishaji, sifa zote kwa pamoja zinamfanya aitwe bilionea.

    MAISHA SIKU CHACHE KABLA YA KIFO
    Habari zinadai kuwa, marehemu alikuwa ndani ya mgogoro wa kifedha na mtu ambaye hakutajwa jina lakini ni wa karibu naye.
    Inadaiwa kuwa, mgogoro huo ni wa muda mrefu na ulikuwa ukisuluhishwa na Dawati la Jinsia, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar.

    SIKU YA TUKIO
    Siku ya tukio inadaiwa marehemu alikuwa Magomeni na watu (idadi yao haikujulikana). Baada ya hapo aliondoka  kwenda kusikojulikana lakini baadaye alimpigia  simu ndugu wa karibu na kumwambia kuwa yuko mahali (hakupataja) ametekwa na sauti anayoitoa inaweza kuwa ya mwisho kisha akakata simu.

    MAELEZO YA POLISI SASA
    Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi Wilaya ya Kisarawe, Desemba 10, mwaka huu,  usiku wa saa nane,  marehemu alionekana akiwa ndani ya gari jeusi umbali wa kilomita saba kutoka Kisarawe Mjini lakini aliondoka baada ya kuliona gari la ‘patroo’ ya polisi.

    Chanzo hicho kikasema kuwa dakika chache mbele polisi waliokuwa katika shughuli za ulinzi usiku huo waliliona gari hilo likienda pembezoni mwa barabara na kupinduka.

    “Tulilifuatilia, tukalikuta limepinduka, ndani ya gari tulimkuta mtu amekufa kwa kujipiga risasi kwani sehemu ya kidevuni na kwenye utosi kulikuwa na tundu la risasi,” kilisema chanzo hicho.

    MAREHEMU ALIDHANIWA MHALIFU
    Habari zinasema katika upekuzi wa awali ambapo polisi walimkuta marehemu akiwa na bastola, risasi 85 na  magazini mbili walidhani alikuwa mhalifu aliyetaka kutekeleza uhalifu mahali ndani ya walaya hiyo.

    NDUGU WA MAREHEMU WANA NENO
    Kwa upande wao ndugu wa marehemu ambao waliomba majina yao yawekwe pembeni, walisema kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu kifo cha ndugu yao huyo kwa sababu hata kifo chake hawakielewielewi.
    Akizungumza kwa hisia ya uchungu, ndugu mmoja alisema katika maisha ya jijini Dar, yeye ndiye baba wa marehemu lakini hakuna alichojua toka kifo hadi kuzikwa.

    Alisema hata mazishi ya marehemu alishtukizwa  kwamba anazikwa siku hiyo jambo lililompa wakati mgumu kufikiria.
     “Sisi kama ndugu wa marehemu, tulipenda akazikwe nyumbani, Makete   (Njombe), lakini ghafla tukaambiwa anazikwa hapahapa Dar tena siku hiyohiyo tuliyopewa taarifa,” alisema ndugu huyo.

    MKE WA MAREHEMU NAYE
    Kwa upande wake mke wa marehemu Zihji alipoulizwa na mapaparazi wetu juzi kuhusu sakata la kifo cha mumewe alijibu kuwa kila mtu anaweza kuongea jambo lolote.

    Aliongeza kusema anachojua yeye ni kwamba kifo cha mumewe kilitokea kama ambavyo mtu mwingine angeweza kufa.

    KAMANDA WA POLISI ANASEMAJE?
    Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, ACP Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa marehemu alikutwa akiwa na jeraha la risasi moja hali ambayo ilionesha alijipiga risasi mwenyewe pengine kutokana na mambo yaliyokuwa yakimsonga kichwani.

    BILIONEA AZIKWA DAR
    Marehemu Muhema alizikwa Desemba 11, mwaka huu kwenye Makaburi ya Sinza jijini Dar. Ameacha mke na watoto watatu wa kike. Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.

    MASWALI TATA
    Kifo cha Muhema kina maswali tata mengi. Kwanza, kama kweli alipanga kujiua kwanini alikwenda mbali na Jiji la Dar es Salaam?

    Pili, kwa nini damu ndani ya gari ilikuwa kidogo wakati uzoefu unaonesha kuwa, mtu anayepigwa risasi ndani ya gari huacha damu nyingi?

    Tatu, ndugu mmoja wa marehemu alikiri kuwa, Muhema alinunua bastola mwaka huu ili kujilinda, sawa kabisa. Je, kwa nini akutwe na risasi nyingi kiasi hicho kama alikuwa anakwenda kufanya uhalifu?

    Nne, ilidaiwa alimpigia simu ndugu mmoja akidai ametekwa na huenda asisikike tena. Polisi walikuta simu kwenye gari lake, kwa nini waseme alijipiga risasi mwenyewe?

    GPL

    Read More »

    Join Swahili One Community, "Like" and you will be one of us forever

    Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
    Copyright © 2013. swahili one Blog - All Rights Reserved
    Customized by: Grace Tommy The One | Powered by: BS
    Designed by: Creative Blogger